skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Adela Madyane- Kigoma

Wavuvi na wachakataji wa mazao ya samaki mkoani Kigoma wameiomba serikali kuwawezesha kutambulika katika taasisi za kifedha ili waweze kuwapatia mikopo itakayowasaidia kutumia vyema masoko ya samaki na dagaa kutoka ziwa Tanganyika nje ya nchi ili kukuza uchumi wao.

Akizungumza Francis John kiongozi wa vyama vya wavuvi mkoani Kigoma na makamu mwenyekiti wa wavuvi Tanzania amekiri juhudi za Rais zitaleta matunda chanya japo bado ipo changamoto ya mitaji kwa wavuvi na wachakataji wengi na kuiomba serikali kuwawezesha kupata mikopo kwa masharti nafuu ili waweze kumudu kasi ya mahitaji ya mazao hayo kwa nchi tofauti tofauti kote duniani.

“ Nchi kama za Marekani, Austaria na Canada wanahitaji dagaa na samaki wa ziwa Tanganyika kwa wingi, kama hatutakopesheka hatutaweza kukidhi haja hiyo,basi serikali ifanye mkakati kupitia wizara ya uvuvi ili wafanyabiashara kutoka nchi hizo waweze kufika Kigoma waangalie namna tunavyochatakata mazao hayo na kufanya makubaliano ya pamoja ili wao wawe wanatuma pesa na sisi tunanunua samaki tunawaagizia, hii itapunguza gharama na kuongeza mitaji yetu” Ameshauri kiongozi wa wavuvi

Bahati Migezo ni mmoja wa wachakataji wa mazao ya uvuvi kutoka mwalo wa Katonga manispaa ya Kigoma Ujiji alisema bado ipo changamoto ya namna ya kuyafikia masoko ya nje na wanaoyafikia ni vishoka ambao hawana leseni ya kupeleka mazao hayo.

“Tunaiomba serikali kupitia mabalozi wake kuweka utaratibu kwa wavuvi na wachakataji kupata leseni ya usafirishaji kwakuwa walionazo si wavuvi halisi, wavuvi halisi wanaonekana kama madalali na vibarua wakati wao ndio wahusika wakuu katika uzalishaji wa mazao hayo na ndio wanaokabiliana na madhara yatokanayo na sekta ya uvuvi,” alisema Migezo

Dagaa wa ziwa Tanganyika wakiwa wameanikwa kwa ustadi katika mwalo wa Kibirizi mjini Kigoma

Naye mvuvi Elias Misubhile kutoka mwalo wa Katonga alisema ili kufanikisha azma ya serikali ya kupanua wigo wa masoko ya samaki nje ya nchi ni lazima kuwe na mikakati ya kuwawezesha wavuvi kupata zana bora za uvuvi zitakazowezesha kupata mazao bora yatakayokidhi vigezo vya biashara kimataifa sambamba na maboresho katika uhifadhi wa mazao hayo ili kuzuia uharibifu.

“Biashara ya kupeleka samaki na dagaa nchi za nje kama Marekani, Australia na Canada haipo wazi, wengi wanaopeleka huko wana ndugu zao na hivyo kunakuwa na mahusiano kati ya waafrika waliopo kule na ndugu walioko huku na sio kwamba zinakwenda moja kwa moja kuingia kwenye masoko, hapana zinalenga watu fulani tu”alifafanua Misubhile

Kwa upande mwingine Selestina Mpelekeza mchakataji na mmiliki wa vyombo vya uvuvi mwalo wa Katonga ameshukuru juhudi za serikali kutafuta fursa za mosoko nchini China na kuiomba wizara kuwafikia ili kubaini changamoto zilizopo kama kikwazo katika kufanikisha biashara hiyo na kuzitatua ili kutoa dira ya namna ya kufika huko

“Hatujui pa kuanzia, waziri wa uvuvi aje atugufungulie mlango, ili tuweze kufika pale serikali inapotaka, asilimia zaidi ya 80 ya wanawake tuliopo kwenye uvuvi hatujui chochote, hatujui mteja tunampataje au anahitaji nini kutoka kwetu, tupo tayari kukua kwaajili ya kulea familia zetu” alisema Mpelekeza

Akizungumzia hilo Patrick Kapungu afisa maendeleo ya biashara kanda ya magharibi kutoka ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) amesema wizara ya mifugo na uvuvi imetenga bilioni zaidi ya 11 kwa mwaka wa fedha wa 2022-2023 kwaajili ya kusaidia wavuvi kupata mikopo ya maboti ya kisasa 160 yatakayosaidia kufanya uvuvi wenye tija ili kuongeza kipato na kupunguza umaskini.

Alisema kwa kanda ya magharibi wameweza kutembelea mikoa ya Kigoma,Katavi na Rukwa na kubaini maombi ya mikopo 63 kwa watu binafsi, makampuni, vikundi pamoja na vyama vya ushirika ambapo Kigoma jumla ya maombi ni 47, Rukwa ni 11 na Katavi ni maombi matano.

“Maombi yote yapo wizara ya mifugo na uvuvi, yatafanyiwa kazi na waliotuma maombi ikiwa wanakidhi vigezo watapewa hizo zana, japo katika maeneo tuliyotembelea tulikutana na baadhi ya maoni kutoka kwa wavuvi kuwa wizara iwatembelee kuona changamoto zaidi zilizopo ili kuzifanyia kazi na kuzitatua na kuleta uvuvi wenye tija” Alisema Kapungu

Naye Abdul Mwilima mwenyekiti wa chemba ya biashara (TCCIA) mkoani Kigoma alisema wapo tayari kuwaunganisha wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi kote duniani cha msingi ni wao kufahamu ubora na uwingi wa bidhaa zinazopatikana.

Mwilima amewashauri wavuvi na wachakataji kujiunga na chemba hiyo ili watambue fursa zilizopo na wanufaike nazo kwakuwa zipo nyingi na zitawanufaisha katika kuboresha biashara na maisha kwa ujumla.

Naye Hashim Muumin mratibu wa mradi wa FISH4ACP alisema wao kama wadau wakubwa katika sekta ya mifugo na uvuvi wataimarisha uchakataji kwa kutumia majiko banifu na kuja namna nzuri ya kuanika dagaa wa ziwa Tanganyika watahakikisha wavuvi na wachakataji wanapata bei nzuri katika masoko ya kikanda ya ndani na ya kimataifa kwa kufanya utafiti na kubaini ubora wa bidhaa wanazotaka na kuwafundisha wachakataji kukabilina na masoko hayo.

Kwa sasa serikali imeweka jitihada katika kufungua masoko ya nje ya nchi ya samaki na dagaa kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan ameweza kufungua soko nchini China ambalo litatoa fursa kwa wafanyabiashara kuuza bidhaa zao lakini bado kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili wavuvi ikiwemo mitaji ili kukidhi vigezo vya masoko hayo.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma