skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na shirika la elimu Sayansi na Teknolojia la umoja wa mataifa UNESCO, zinaonesha kuwa waizraeli wanasoma wastani wa vitabu 64 kwa mwaka, Wajapani vitabu 40, wamarekani vitabu 21 na wafaransa wanasoma wastani wa vitabu 20.

Tanzania ilifikia kiwango cha juu cha usomaji wa vitabu katika miaka ya 1970, lakini kwa sasa idadi hiyo imepungua kwa kiwango kikubwa.

Wasomi wanaeleza kuwa kujisomea vitabu kuna manufaa mengi katika jamii yoyote ile ikiwamo kusaidia katika mabadiliko ya tabia na kuwa na kizazi bora, pia inaongeza kichocheo cha kasi katika kupata maendeleo, ujuzi na utaalam mpya.

Kwa nchi za Afrika usomaji wa vitabu ni utamaduni ambao haujazoeleka, na hata watu walio nunua vitabu ukiwauliza lini wamevisoma wataeleza sababu nyingi zilizopelekea wakiashindwa kuvisoma.

Dkt. Kamfipo Gidioni ni Amidi Mshiriki Chuo Kikuu cha Dar es salaam, shule kuu ya uandishi wa habari na mawasiliano kwa umma, anakiri kuwa ni kweli watanzania hawapendi kusoma vitabu na chanzo ni malezi ya kiutamaduni.

Amesema tabia hiyo imezalisha usemi ndani ya jamii kuwa ukitaka kumficha jambo Mwafrika basi jambo hilo liweke katika maandishi, hivyo ili kukabiliana na changamoto hiyo jamii inapaswa kuwakuza watoto katika mazingira ya usomaji wa vitabu.

Hakuishia hapo  Gidion, ameongeza kuwa tatizo la kutosoma vitabu kunaweza kusababisha tatizo la Afya ya akili, kuwa na vijana wasio na maarifa nataifa kuendelea kusuasua kutokana na kukosa vijana wenye weledi.

“Taifa la watu wasio penda kusoma vitabu linaweza kuwa na watu wenye matatizo ya afya ya akili, lakini pia linaweza kuchelewa sana katika kupata maendeleo kutokana na kukosa vijana wenye maarifa”, amesema Gidion.

Mashirika mbalimbali yameanzishwa likiwemo shirika lisilo la kiserikali SOMA lenye lengo la kuhamasisha usomaji wa vitabu, Magdalena Thomasi ni Meneja Mradi wa shirika hilo, anasema sio kweli kwamba watanzania hawapendi kusoma vitabu bali, tatizo ni kukosekana kwa maeneo toshelevu ya kusomea yaani maktaba.

Jamii zinapaswa kurejesha utamaduni wa kusoma vitabu kwa ustawi wa kizazi chenye ustadi.

“Waandishi wachache ambao vitabu wanavyoandika vikishuka kimauzo basi wanaibuka na kuaminisha jamii kuwa watanzania hawapendi kusoma vitabu, sio kweli ingekuwa ndivyo basi hata magazeti yangekuwa hayanunuliwi, watu wanasoma sana isipokuwa inatengemea wanataka kusomama nini kwa wakati huo”, amesema Magdalena.

Hata hivyo muandishi wa kitabu cha Mariam, Gwantwa Lucas, binti anayeamini katika uandishi wa vitabu na uchoraji wa katuni anasema vijana wengi hasa wakike hawapewi muda wa kutosha kupumzika na kujisomea vitabu.

“Kazi nyingi za nyumbani wanazopewa watoto hasa wakike wanapotoka shuleni zinachangia sana kuminya muda wao wa kujisomea vitabu, hii inasababisha wazazi kuwawekea mipaka watoto wao katika kujiendeleza kwa madai ya kuwafundisha kazi”, amesema Gwantwa.

Haya tujiulize ni lini mara ya mwisho, ulinunua kitabu kwa lengo la kukisoma? na je uliponunua kitabu hicho ulikisoma? Au hujawahi kabisa kuchukua kitabu na kujisomea ukiamini huna muda wa kufanya hivyo kutokana na majukumu mengi ya kujitafutia mkate wa siku au unaamini kuwa ulisha maliza muda wa kujisomea vitabu baada ya kuhitimu masomo yako

Mwandishi:Mussa Mkilanya

Mhariri: Adela Madyane

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma