skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limetoa misaada mbalimbali kwa ajili ya wafungwa katika magereza matatu ya mkoa wa Kigoma kama sehemu ya mpango wake wa kuunga mkono serikali katika maeneo yanayohifadhi wakimbizi

Msaada huo umetolewa mapema jana ambapo Magereza yaliyonufaika ni Bangwe, Kwitanga na Ilagala ambako msaada uliotolewa ni pamoja na Magodoro 60 kwa kila gereza, mablanketi 200 kwa kila gereza, sabuni za kufua na kuogea, mafuta ya kupaka, dawa za meno pamoja na mafuta ya kuzuia mbu vyenye tahamani ya shilingi za kitanzania milioni 27

Akiongea wakati wa utoaji wa msaada huo mkuu wa kitengo cha ulinzi wa mkimbizi wa UNHCR mkoani Kigoma Bw. Peter Muriuki alieleza kuwa, UNHCR katika mipango yake ya ushirikiano baina yake na serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo, imekuwa ikitoa misaada ya kiutu kwa wakimbizi pamoja na kwa jamii ya maeneo yanayohifadhi wakimbizi hao ikiwemo mkoa wa Kigoma

Muriuki alibainisha kuwa katika idara ya magereza UNHCR imetoa misaada mbalimbali ya kuwezesha masuala ya utawala ikiwemo zana za TEHAMA kama vile computa na mfumo wa mawasiliano, na kwamba utoaji wa misaada hiyo ni pamoja na kutambua kuwa ndani ya Magereza wapo pia wakimbizi na raia wengine wa kigeni ambao wanahitaji huduma za kijamii kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki

Shehena ya msaada kwa wafungwa uliotolewa na UNHCR mkoani Kigoma katika magereza ya Bangwe, Kwitanga na Ilagala. Picha na Prosper Kwigize

Kwa upande wake mkuu wa gereza la Kwitanga Kamishna msaidizi wa magereza Dr. Uswege Mwakahesye amekiri kuwa kama ilivyo kwa huduma nyingine za kijamii, magereza pia hukumbana na changamoto nyingi zinazohitaji wadau wengine kuchangia ikiwemo miundombinu na huduma nyingine za kiutu.

Naye kaimu mkuu wa gereza la kilimo la Ilagara wilayani Uvinza Mkaguzi wa magereza Charles John Sinzira amekiri kuwa msaada huo wa UNHCR umeletwa kwa wakati kutokana na ukweli kwamba magereza nyingi za mkoani Kigoma zinahifadhi na kurekebisha tabia za wafungwa wengi kutoka nchi za Jirani, wengi wao wakitokea nchini Burundi.

Picha ya Pamoja ya maafisa wa UNHCR na maafisa wa magereza katika Gereza la Ilagala baada ya kupokea vifaa. Picha na Prosper Kwigize

Inaelezwa kuwa wafungwa wengi ambao ni raia wa nchi nyingine hukabiriwa na uhaba wa mahitaji mbalimbali kutokana na kutokuwa na nduguu wa karibu wa kuwatembelea na kuwapa Faraja kama ilivyo kwa wafungwa watanzania ambao hutembelewa na ndugu zao chini ya utaratibu maalumu wa kimagereza.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma