skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

MRATIBU mkazi wa umoja wa mataifa nchini ndugu Zlatan Milisic ameahidi kuendelea kuunga mkono shughuli na miradi ya maendeleo katika maeneo yanayohifadhi wakimbizi sambamba na kwa wakimbizi wenyewe.

Miradi ya kipaumbele ambayo amethibitisha kuendelea kutoa usaidizi ni pamoja na nyanja za uwezeshaji vijana na wanawake kiuchumi, kupinga ukatili, huduma za maji, mazingira, kilimo na afya kupitia mradi wa pamoja Kigoma unaoundwa na mashrika 16 ya umoja wa mataifa.

Mheshimiwa Zlatan ameyasema hayo baada ya kutembelea wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma na kukagua miradi mbalimbali inayofadhiliwa na program ya pamoja Kigoma akiwa na viongozi wengine wa jumuia ya Ulaya ambapo amesema lengo la mpango huo ni kusaidia maendeleo ya wakimbizi na wananchi wenyeji kwa kusaidia juhudi za Serikali kuimarisha njia za watu kujipatia maendeleo kwa kushirikiana na mashirika hayo yakiongozwa na shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi 

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu amesema uwepo wa miradi inayosimamiwa na jumuia ya Ulaya kupitia mashirika 16 ya umoja wa mataifa umewezesha kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Wananchi katika kijiji cha Muzye wilayani Kasulu ambao wamenufaika na mradi wa jengo la huduma ya uzazi na vifaa tiba wamesema mradi huo umepunguza madhara ya vifo kwa akina mama na watoto baada ya kuanza kujifungulia katika zahanati hiyo kufuatia kuboreshwa kwa huduma na uwepo wa vifaa.

Sikiliza ripoti iliyoandaliwa na mwandishi wetu Kadislaus Simon

Kigoma ni miongoni mwa maeneo machache barani Afrika yanayohifadhi wakimbizi wengi kutoka nchi za Burundi na DRC

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma