skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki,Bariadi.

Wananchi wa kata ya Bunamhala wilayani Bariadi mkoani Simiyu wameishukuru serikali kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) kwa kuwajengea nyumba kwa ajili ya watumishi wa zahanati iliyopo kwenye kata yao.

Wamesema hayo baada ya uzinduzi wa miradi inayotekelezwa na TASAF uliofanyika kwenye zahanati ya Imalilo iliyopo kata ya Bunamhala wilayani Bariadi huku   wakiongeza kuwa  ujenzi wa nyumba hiyo utawawezesha watumishi kuwa jirani na zahanati hiyo.

 “tunashukuru kwa kutuletea zahanati na sasa tunaona ujenzi wa nyumba ya watumishi umeanza, nyumba hii itatusaidia sana maan kwasas ikifika usiku huduma hakuna maan wataalamu wetu wanakaa mbali, na ugonjwa hauna muda”Joyce Salamba mkazi wa Imalilo

“Wanalala mbali usiku ukipata mgonjwa mfano mama mjamzito huwezi kumleta hapa( zahanati) lakini wakijenga nyumba karibu ni rahisi kupata huduma si tutakuwa tunajua wanakaa wapi ombi ujenzi ukamilike mapema”Ester Mashala mkazi wa Imalilo.

Mkuu wa wilaya ya Bariadi ndugu Simon Simalenga akishiriki kazi ya uchimbaji wa msingii wa ujenzi wa zahanati

Andrew James ni  mganga mfawidhi  wa zahanati ya Imalilo inapojengwa nyumba ya watumishi  amesema  nyumba hiyo ikikamilika  itasaidia huduma kwenye zahanati hiyo kufanyika muda wote( saa 24) na  wananchi watapata huduma kwa wakati,kwani katika zahanati wanapokea hadi akina mama wanaofika kujifungua na katika kujifungua hakuna muda maalum.

“tunaishukuru TASAF kwa kuweza kutujengea nyumba ya watumishi, nyumba hii ni njia mojawapo ya kuboresha huduma za afya kwasababu watumishi wanapoishi mbali na zahanati  maana yake kuna huduma ya nje ya muda wa kazi saa 9:30 wananchi wanazikosa lakini kukiwa na nyumba eneo la kazi maana yake huduma zitakuwa muda wote ”

Bonyeza Picha hii hapo juu usikie nini kilisemwa na mganga mkuu pamoja na wananchi wa Mji wa Bariadi

James amesema  zahanati wanapokea hadi akina mama wanaofika kujifungua na katika kujifungua hakuna muda maalum lakini kwasasa wakina mama hao na wagonjwa wengine wanapata changamoto endapo watahitaji huduma usiku kwani kwasasa watoa huduma kwenye zahanati hiyo wanaishi nje ya kituo cha kazi.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Bariadi Adrian Jungu amesema halmashauri hiyo imepata shilingi milioni 731 kwaajili ya utekelezaji wa miradi minane  kwenye kata mbalimbali, baada ya utekelezaji mzuri wa miradi iliyopita ambapo timu ya TASAF  ilifika nakuridhika na utekelezaji na hivyo kuipatia fedha hiyo huku mwenyekiti wa halmashauri hiyo Elias Masanja akisema fedha hiyo itasimamiwa kikamilifu  ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Awali akisoma taarifa mbele ya mkuu wa wilaya ya Bariadi ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa utekelezaji wa miradi ya kuondoa umasikini kwa kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu katika halmshauri ya mji wa Bariadi mratibu wa TASAF kwenye  halmashauri ya mji huo Omary Massumo ametaja mikakati ya utekelezaji ambapo amesema wataendelea kushirikiana na kamati za mitaa, kamati za usimamizi jamii ili  kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu matumizi ya vifaa vya ujenzi na utendaji wa mafundi wa kila siku.

Mbali na hayo amesema wataendelea kufanya ufatiliaji  wa mara kwa mara kuhakikisha shughuli zinafanyika kama zilivyokusudiwa, manunuzi yanafanyika kwa kuzingatia miongozo ya manunuzi na kufuata uhalisia wa bei zilizopo sokoni kabla ya kupitisha malipo ikiwa ni pamoja na timu ya uhandisi kutembea mara kwa mara kuona  majengo yanayojengwa kama yamefuata ramani na michoro ya majengo  ili kama kuna kasoro zirekebishwe mapema.

Akizindua utekelezaji wa miradi ya kuondoa umasikini kwa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya tasaf katika halmshauri ya mji huo hiyo mkuu wa wilaya ya Bariadi Simon Simalenga amesema nia ya serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma huku akitoa wito kwa kamati husika kusimamia ujenzi wa ipasavyo na yeye atafatilia kwa ukaribu kila mradi wilayani hapo.

Miongoni mwa zahanati ambazo zinazoenda kunufaika na miradi hiyo kwenye halmashauri ya mji wa Bariadi ni pamoja na Imalilo,Nyakabindi,Mitale,Bipyayi na Gisadi

 

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma