skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Adela Madyane-Kigoma.

Wafanyabiasha wa dagaa na samaki katika soko la mwalo wa kibirizi, manispaa ya Kigoma ujiji, wameshusha bei ya mazao hayo kutoka sh 40,000 iliyodumu kwa takribani wiki mbili zilizopita hadi sh 20,000-30,000 kwa kilo baada ya serikali kutoa tamko la kutokusitisha shughuli za uvuvi za ziwa Tanganyika.

Madai ya kufungwa kwa ziwa hilo kulisababisha kuadimika sokoni mazao ya uvuvi kwa kile kinachodaiwa baadhi ya wafanyabiashara wakubwa kununua mazao hayo kwa wingi na kuyahifadhi ndani ili waweze kuuza kwa bei ya juu endapo ziwa hilo lingefungwa mnamo Mei 15,2023.

Wakizungumza wafanyabiashara na wachuuzi wa samaki na dagaa mwaloni hapo wamesema wamefurahishwa na tamko la serikali la kutozuia shughuli za uvuvi na kusema kuwa mzunguuko wa uuzaji wa mazao hayo umeanza kuongezeka na kuisihi serikali kufanyia kazi vyanzo vya uvuvi haramu.

Tatu Musa ni mchuuzi wa dagaa katika mwalo huo, amesema dagaa zimeongezeka sokoni na anauza kilo moja kwa elfu 25,000 na kwamba sasa anapata wateja wa kutosha kinyume na ilivyokuwa ambapo watu wengi walishindwa kununua dagaa kutokana na kuwa na bei ya juu na kuiomba serikali kuondoa sokoni nyavu za free mire na ringnet ambazo ndizo kisababishi kikuu cha uvuvi haramu.

Akiongeaea Felister Paulo amesema wiki iliyopita waliuza dagaa kwa elfu 38,000-40,000 hali iliyosababisha mzunguko hafifu kibiashara na kwamba kazi hiyo ilianza kuwa ngumu kwao na baadhi yao walianza kuiacha na kuishukuru serikali kurejesha kazi yao maana wangeishi maisha magumu kwakuwa wao kama akina mama ndio wenye majukumu zaidi ya kulea familia.

Samaki aina ya Mgebuka kutoka Ziwa Tanganyika zikiwa katika Soko la Samaki la Kibirizi

Naye Ramadhani Adam amesema dagaa zitaendelea kushuka au kupanda kutokana na hali ya ziwa kwani ziwa huwa linajifunga na kujifungua lenyewe na kwamba kwa mwezi wa sita hadi wa saba ziwa huwa linajifunga na kusababisha uchache wa samaki na dagaa hivyo ni vyema watu wakanunua dagaa kipindi hiki ambako zimetolewa stoo na kushuka bei.

Kwa upande wa Khatib Hussein mfanyabishara mkubwa wa samaki na dagaa amesema yeye alifanikiwa kuhifahi takribani kilo 200 za dagaa ambazo alitarajia kuziuza mwezi wa pili wa kuzuiliwa kwa shughuli za uvuvi ili kujipatia faida mara dufu ila sasa imebidi aziuze ili kuendana na hali ya soko.

Naye Kagoma Idd amekiri kuwa tamko la serikali la kutozuia shughuli za uvuvi litawaathiri baadhi ya wafanyabiashara wakubwa kwani hata yeye alitunza kilo 300 kwaajili ya kuuza baadae na kuona ni vyema hasara ipatikane kwa watu wachache kuliko kuwaathiri watu wengi.

Hata hivyo Salim Ahmed ameomba serikali ikishirikiana na wataalamu kuhakikisha wanakabiliana na uharibifu wa mazingira uliopo ziwani, kutafuta namna za kukabiliana na madiliko ya tabia nchi sambamba na kumaliza changamoto za uvuvi haramu hasa maeneo ya pori ambako hakuna usimamizi na watu kufanya uvuvi holela.

Tanzania ilidai kutekeleza makubalianao ya rasimu ya kusimamishwa kwa shughuli za uvuvi wa ziwa Tanganyika kwa kipindi cha miezi mitatu ikiwa ni makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha mwaka 2022 na nchi nne zinazozunguka ziwa hilo ambazo ni Zambia,Tanzania,Burundi na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC).

Nchi hizo zilikubaliana kanuni moja ya kutambua zana haramu za uvuvi ili kurusu mazalia ya samaki kwa wingi na kudhibiti uvuvi haramu, uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma