Na. Irene Bwire -PMO na Anita Balingilaki Buha - Simiyu WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka…
Na. Matinde Nestory – Mwanza
Jamii imeshauriwa kubadilika na kuonesha mfano bora kwa watoto wenye ulemavu hususani mwenye changamoto ya akili kwa kuwatendea mema hali ambayo itasaidia watoto hao waige jinsi ambavyo watu wazima wanavyoishi.
Hayo yamebainishwa Leo na Afisa Maendeleo wilaya ya Ilemela Sara Nthangu wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya ujuzi kazi kwa watoto wenye ulemavu iliyofanyika Lumala wilaya ya Ilemela Mkoa wa Mwanza.
Bi Nthangu amesema kuwa jamii inatakiwa ibadilike kwa kuwaonesha upendo watoto hao hali ambayo itapelekea kuwajengea uwezo wa kujifunza pamoja na kujitambua.
“Serikali imeboresha mazingira kwa watoto wenye ulemavu ambapo wanapata elimu jumuishi na pia serikali iliona ni bora Sasa badala ya kuwatenga kuwa na shule zao peke Yao wawe na wenzao ili waweze kujichanganya kule kutamfanya mtoto mwenye ulemavu kuelewa mazingira kwa haraka”amesema Bi Nthangu.

Ameongeza kuwa watoto wenye ulemavu wasitengwe waendelee kuwekwa kwenye vitengo maalum kwenye shule za kawaida hii itasaidia kupunguza unyanyapaa kwa watoto wenye mahitaji maalumu.
Aidha amesema kuwa wazazi wasiwafiche na kuwatenga watoto wenye mahitaji maalumu hii itasababisha kuwaongezea ulemavu.
“Mtoto ukimtenga na wenzake kwa kumfungia ndani unampotezea fursa ya kujifunza na kujichanganya sababu umri wa utoto ndio umri wa kujifunza,ukimtenga unampotezea muda wa kujifunza namna ya kushi na binadamu wenzake”amesema Bi Nthangu.
Kwa upande wake mkurugenzi wa shirika la Action For Community Development (ACODE) Winner Chimba amesema kuwa kupitia shirika hilo ambalo linajihusisha na mradi wa binti mwerevu pamoja na tiba tengamao kwa watoto wenye ulemavu kwa kuwapa ujuzi kazi hususani wenye matatizo ya akili.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo ambayo yamechukua takribani wiki tatu yakiwa na lengo la kuwasaidia watoto wenye ulemavu kujifunza ujuzi mbalimbali ikiwemo kufuma,kutengeneza Maua ,kuosha miguu na stadi kazi ambazo zitawasaidia kujitegemea.
“Tuliona tuwe na mafunzo hayo wakati wa likizo kwa watoto wenye ulemavu ili nao waendelee na masomo kipindi Cha likizo sababu kundi hili huwa linasahaulika na watoto kubaki mtaani wakizurura”amesema Bi Chimba.
Ameongeza kuwa wamekuwa na watoto 10 kwa kuanzia wenye ulemavu wa akili,uziwi na kutoweza kuzungumza pamoja na down syndrome ambao ujunzi huo utawasaidia hata Kama asipoweza Kupata elimu katika mfumo rasmi.
Aidha amewataka wazazi kuacha kuwaficha watoto wenye ulemavu kwa kutowapa Elimu na kuwaona ni mkosi katika familia hali ambayo inatishia maisha ya watoto hao.
Hata hivyo katika hitimisho ya mafunzo hayo zawadi mbalimbali zimetolewa ikiwemo madaftari,kalamu pamoja na kitenge kwa ajili ya kuwajengea uwezo watoto hao.
Nae mmoja wa Wadau wa maendeleo ya watoto Adelina Nkwabi kutoka shirika la Beyond Giving Tanzania akielezea changamoto amesema kuwa uelewa kwa jamii kuhusu ulemavu pamoja na wazazi wenye watoto wenye ulemavu hawaelewi ambapo jamii inajua baadhi ya ulemavu ambao unaonekana.
Ameeleza kuwa jamii haina uelewa juu ya elimu inayohusiana na ulemavu pamoja na Idara ya afya bado haijabainisha kwa wazazi changamoto ambazo wanaziona kwa Mara ya kwanza kwa watoto hii inapelekea mzazi analea mtoto wake bila kujua shida ni nini.
Sanjari na hayo amesema kuwa Taasisi zinazoshughulikia masuala ya afya waweke mtaalam kwenye clinic ambapo mzazi anaweza Kupata elimu juu ya ulemavu na jinsi ya kumuhudumia mtoto mwenye ulemavu.
Hata hivyo ameiomba jamii kuendelea kuhamasisha akina baba kutokimbia familia zao hali ambayo itasaidia kupunguza ukatili kwa watoto wenye ulemavu.
Kwa upande wake Mwalimu wa watoto wa vitengo maalum Hollo Bukombe amesema kuwa watoto hao wamekuwa wakifundishwa vitu vya mwanzo ikiwemo kupiga mswaki,kunawa uso,kula pamoja na kwenda chooni.
Ameongeza kuwa wazazi wanapowaleta watoto shule wanawajengea uwezo wa kujifunza stadi mbalimbali za Kazi pamoja na kujichanganya na watoto wengine.
Nae mmoja wa wawakilishi wa wazazi wa watoto wenye ulemavu Modester Lucas amesema kuwa changamoto ni uangalizi wa karibu,namna ya kuwachanganya watoto wenye ulemavu na watoto wenzao ambao wanatakiwa wawatazame mtazame chanya pamoja na kujifunza kwa shida.