skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Matinde Nestory, Mwanza

Shirika lisilo la kiserikali Beyond Giving Tanzania limetoa msaada wa Televisheni yenye thamani ya shilingi 450,000 katika shule ya Msingi Wita yenye kitengo Cha Elimu maalum cha wanafunzi wenye ulemavu katika kata ya kisesa wilayani Magu.

Akikabidhi msaada huo, mkurugenzi wa shirika hilo Bw. Joseph Msuka amesema leo la kifaa hicho cha mawasiliano ni kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu kujifunza kwa vitendo, kuwaweka pamoja wanafunzi wenye ulemavu na wanafunzi wasiokuwa na ulemavu, kuongeza ufanisi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, pamoja kuburudika kwa kutazama michezo mbalimbali.

Msuka ameongeza kuwa mtoto mwenye ulemavu ni sawa na mtoto mwingine katika kuwapatia Elimu na Afya (Matibabu) na kuitaka jamii kuondoa dhana ya mtoto mlemavu ni mkosi au laana katika familia.

Akizungumzia changamoto amesema wanafunzi wenye ulemavu wamekuwa hawashirikishwi katika masuala mbalimbali ya kijamii na kwamba wengi wao wanakosa haki ya elimu kutokana kufichwa na kaya zao, umbali wa vijiji wanavyoishi, upungufu wa vifaa vya kujifunzia pamoja na miundo mbinu ambayo sio rafiki kwa watoto wenye ulemavu.

“Jamii inayoishi na watoto wenye ulemavu isiwafiche bali iwatoe hadharani wapelekwe shule ili waweze kujifunza Elimu ya darasani na ya vitendo ambayo itawasaidia wao na jamii kwa ujumla”amesema Msuka

Kwa upande wake Afisa Elimu kata ya Kisesa Deogratias Lwanga ambaye alikuwa mgeni rasmi katika makabidhiano hayo, amesema kuwa Televisheni hiyo itawasaidia kuboresha vipaji vya kuimba na vipaji vya kucheza,pia itasaidia kupunguza ubaguzi kwa kuwaweka pamoja watoto wenye ulemavu na watoto wengine pamoja itasaidia kufundisha na kujifunzia standi mbalimbali za kazi.

Aidha ameziomba Taasisi binafsi,Serikali na mashirika kujitokeza kuwasaidia watoto wenye changamoto ya ulemavu kwa kuwapatia huduma ya kielimu kwa kuwapatia vifaa vya kujifunzia pamoja na huduma ya kiafya.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Wita Said Joseph amesema msaada huo utasaidia wanafunzi wenye ulemavu wa akili kujifunza kwa vitendo ambapo watajifunza kwa ufanisi.

Mwl Joseph amekiri kuwa ipo changamoto ya vifaa vya kufundisha na kujifunzia  kwa walemavu wa akili, vifaa vya kuhifadhia vitu, Chumba Cha kulia chakula pamoja na upungufu wa madarasa.

Shule ya msingi Wita ina wanafunzi 51, wanafunzi wa kike 26 na wanafunzi wa kiume 25 ambapo Kuna makundi mawili ulemavu wa akili na ulemavu wa kusikia na kuona pamoja na Walimu wanne (4) wa Elimu Maalumu

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma