skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Serikali ya Burundi imeihakikishia Jumuiya ya Afrika mashariki kuwa nchi yao iko salama na inawakaribisha wawekezaji katika sekta mbalimbali kwenda kufanya biashara na nchi hiyo ambayo imekuwa katika machafuko ya kisiasa na kikabila kwa Zaidi ya muongo mmoja.

Hayo yamebainishawa na Rais wa Burundi Everist Ndayishimiye ambaye yuko nchini Tanzania kwa ziara ya siku moja ambapo anakutana na Rais Dr. John Magufuli katika mji wa Kigoma magharibi mwa Tanzania.

Rais Ndayishimiye amebainisha kuwa baada ya kumalizika kwa uchaguzi uliofanyika kidemokrasia, serikali yake ilikaa na pande zote za kisiasa na kukubaliana kuhakikisha nchi haiendelezi migogoro, sambamba na kufuta dhana za makabila ya watusi na wahutu na kukubaliana kuwa Burundi ina kabila moja tu ambalo ni warundi.

Sisi ni warundi, tunaongea lugha moja, hakuna sababu ya kuendelea kutambua makundi ya wahutu na watus kama makabila, kabila yetu ni warundi na lugha yetu ni Kirundi, Wazungu walitumia ukabila kutugawanya ili kututawala, sasa tunajitambua kama taifa huru” amesema Rais Ndayishimiye

Aidha Burundi kupitia kwa Rais wake imeishukuru Tanzania kwa kuendelea kuwahifadhi wakimbizi wa Burundi sambamba na kuwapatia Uraia wale waliopenda kubaki Tanzania baada ya kuishi kwa miaka 40 ambapo Tanzania ilitoa vyeti vya uraia kwa wakimbizi wapatao laki moja na sitini elfu waliokuwa katika kambi na makazi ya Mishambo, Katumba na Ulyankuru katika mikoa ya Katavi na Tabora.

Amepongeza pia kuwepokwa mkakati wa kuunganisha Burundi na mfumo wa usafiri wa Anga, majini na nchi kavu kwa njia ya reli inayotarajiwa kujengwa kutoka Uvinza Tanzania hadi makao makuu ya nchi ya Burundi -Gitega.

Akihutubia wananchi wa mji wa Kigoma Rais Ndayishimiye amesema kuwa Tanzania ni Mzazi wa Burundi na kwamba undugu uliopo ni wa kihistoria na inatakiwa uanze kutumika katika ukuzaji wa uchumi na usalama kwa pande zote mbili, huku akisisitiza watanzania kuwaamini warundi.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma