skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Kwa wakongwe wa siasa mkoani Kigoma hasa minyukano ya chama tawala na Upinzani katika majimbo ya Kigoma kusini na hata Kigoma mjini huwezi kuacha kumfahamu Optatus Likwelile, msomi na mwanaharakati mwenye mvuto kwa vijana.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 Likwelile ni miongoni mwa wanasiasa waliojitokeza kuwania uteuzi wa CCM kugombea Ubunge katika jimbo la Kigoma kusini, akiomba ridhaa ya kwenda kutwangana na Kafulila pamoja na Kifu Gulam Huein waliokuwa wakiwika katika siasa za mageuzi.

Hata hivyo Likwelile ambaye alikuwa Kiongozi wa Shirika la Action Aid aliloliongoza kwa miaka kadhaa na kutekeleza miradi mingi ya maendeleo hasa katika sekta ya elimu, mazingira na afya ambao walijikita zaidi katika vijijin vya mwambao wa ziwa Tanganyika kusini mwa mji wa kigoma na kuanzisha ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu, hakuteuliwa na chama cha mapinduzi na hivyo kuamua kukipa kisogo chama tawala na kuhamia Upinzani katika chama cha wananchi CUF ambako walimpokea kwa vifijo na kumteua kuwania Ubunge, hata hivyo hakufaulu baada ya Kafulila kulitwaa jimbo hilo.

Kwa mujibu wa Likwelile, kilichomkimbiza CCM na kujiunga CUF ni kila alichokitaja kuwa CCM alichezewa faulo kwa kumnyima uteuzi na kuwapa kipaumbele ambao yeye aliamini hawakuwa na mchango wowote kwa chama hicho wala kwa maendeleo ya mkoa wa Kigoma hususani Jimbo la Kigoma kusini ukilinganisha na alivyokuwa yeye.

Katika maelezo yake Likwelile anasema aliamua kusalia upinzani kwakuwa hakukuwa na kiongozi au mbunge ndani ya mkoa wa Kigoma aliyeonesha mapenzi makubwa kwa mkoa hadi alipomfahamu Profesa Joyce Ndalichako ambaye ni mbunge wa Jimbo la Kasulu mjini.

Sikuwahi kumuona Mama Ndalichako zaidi ya kusoma habari zake katika vitabu na magazeti, habari zake zilisambaa zaidi wakati wa uchaguzi mkuu 2020, hata hivyo nilikuwa nikifuatilia nyendo zake na uchapa kazi wake tangu akiwa Chuo kikuu, baraza la mitihani Tanzania na baadaye akiwa waziri wa elimu baada ya kuteuliwa na Rais hayati Magufuli kuwa mbunge na kisha kumpa Uwaziri wa elimu, misimamo yake, uchapakazi wake ulinivutia sana, na binafsi namuona kama mkombozi wa Kigoma” Anasema Likwelile

Likwelile ambaye ameongoza mashirika kadhaa ya kijamii kitaifa na kimataifa hivi karibuni alistaafu kazi katika chama cha msalaba mwekundu ambako alihudumu kama afisa mwandamizi mkoani Kigoma katika miradi ya huwahudumia wakimbizi wa Burudi na DRC na kisha kuamua kuufanya mkoa wa kigoma hususani mji wa Kasulu kuwa nyumbani kwake rasmi.

“Mimi ni mzaliwa wa Ifakara lakini nimeamua Kasulu ndiyo pawe nyumbani, nilitamani kwa miaka mingi kukutana na profesa Ndalichako kutokana na alivyonivutia kutokana na uchapa kazi wake, sasa leo nimemuona, nimeushuhudia uwezo wake wa kutengeneza agenda na pia kufanya jambo kwa wakatii na kwa kuzingatia maslahi ya Kasulu na mkoa wa Kigoma, na sasa kwa heshima yake natamka rasmi kuwa naachana na CUF na niko tayari kujiunga na CCM kama asante kwa mama Ndalichako” Anasisitiza Likwelile akionesha hisia za hali ya juu.

Uamuzi wa Likwelile kukipenda upya Chama Cha Mapinduzi ulikuja hivi Karibuni alipokutana na Profesa Joyce Ndalichako wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi katika Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Radio cha Buha FM kinachojengwa mjini Kasulu ambacho kinatarajiwa kusikika mkoa mzima wa Kigoma.

Profesa Ndalichako akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha radio cha BUHA mjini Kasulu

Likwelile anasisitiza kuwa Chama cha mapinduzi kinapaswa kujivunia kuwapata akina mama wenye uchungu na wananchi huku akimtaja Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuwa dira sahihi ya kuwajengea uwezo wanawake kwa kuwapa fursa za uongozi, na kwamba wote aliowapa nafasi ni dhahiri wamefanya ambayo wanaume wengi walishindwa hasa katika nafasi za Ubunge na Uwaziri.

Kwa upande wake Profesa Ndalichako alimshukuru Likwelile kwa heshima kubwa kwa chama cha mapinduzi na kwa kuamua kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kukijenga chama na serikali kwa maslahi ya watanzania, na kumtaka afuate taratibu za kupata kadi ya CCM na kuwa mwanachama upya baada ya kuishi katika itikadi za upinzani kwa zaidi ya miaka 10.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kasulu Mheshimiwa Abdallah Mbelwa Chidebwe ambaye pia alikuwa shuhuda wa tukio hilo, alifurahishwa na azimio la Likwelile kurejea CCM na kuahidi kuandaa utaratibu maalumu wa kumpokea ndani ya chama tawala.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma