Na. Mwandishi wetu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip…
Adela Madyane-Kigoma
Wananchi wa kijiji cha Kigembe wilayani Kasulu mkoani Kigoma wameishukuru serikali kufuatia kijiji chao kujengewa mradi wa Maji ambao umetengeneza historia mpya katika kijiji hicho kilichokosa huduma hiyo kwa miongo kadhaa
Kijiji hicho kilichopo umbali wa kilomata 50 kutoka wilayani Kasulu kilinzishwa mwaka 1976, kilikuwa na historia ya ugumu wa upatikanaji wa maji safi na salama hadi kufikia Mei 2021 ulipoanzishwa ujenzi wa mradi wa maji chini ya ufadhili wa shirika la kimataifa la maendeleo ya serikali ya Uingereza uliogharimu zaidi ya Tsh milioni 339
Wakizungumza na BUHA FM baadhi ya wanachi wametoa hisia zao za kukabiliana na changamoto ya maji kwa muda mrefu wakitaja kuwa moja ya mambo yaliyozorotesha maendeleo ya kijiji chao ni ukosefu wa maji ya uhakika.
“Kwa muda mrefu hapa kijijini kwetu, wanawake na watoto walikuwa wahanga wa upatikanaji wa maji ikiwa ni pamoja na kuchelewa kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo kama kuchelewa kwenda shuleni, shambani na wengine kupata matusi na waume zao” amesisitiza Wilbrada Sheba mkazi wa Kigembe

“Tulitembea umbali mrefu kutafuta maji, na ilituchukua muda mrefu si chini ya dakika 30 kufika kwenye chanzo cha maji, na tukifika tunalazimika kusubiri kama dakika nyingine 30 na hata zaidi kulingana na msimu, ilituchelewesha kufanya shughuli nyingine kwa wakati” ameongeza Bw. Sheba.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kitongoji cha Mumtundu katika kijiji cha Kigembe Johari Bakari alisema wamekuwa wakitegemea maji ya kuvuna ya mvua, mito na madimbwi na hali kuwa ngumu wakati wa kiangazi ambapo madimbwi mengi yanakauka na baadhi ya mito kupunguza ujazo wake na hata kukauka.
“Tulitumia maji eneo moja na mifugo kwakuwa hakuna eneo maalumu la kunyweseha mifugo isipokuwa katika maeneo ambayo pia tunachota maji kwa matumizi ya nyumbani, tulipata na magonjwa ya matumbo kwasababu hiyo, tunaishukuru serikali kwa kutusaidia kupata maji,” alisema Bakari.

Kwa upande wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) meneja wa wilaya ya Kasulu Edward Kisalu alisema, mpaka sasa Mradi huo umekamilika kwa zaidi ya asililimi 97 na unahudumia wananchi wapatao 4874 ambao utaongeza asilimia 0.93 katika asilimia ya upatikanaji wa maji katika wilaya ya Kasulu na kufikia aslimia 67.8
Kisalu amezitaja changamoto kuwa ni upatikani wa pump na sola ili mradi huo kufikia asililimia 100 za ufanisi wake na kwamba kwa sasa mradi unatumia jenereta kutoka wilaya ya Kakonko kwa muda, una tanki la maji lenye ujazo wa lita 100,000 pamoja na bomba 9 za maji za jamii zilizopo ndani ya kijiji ambazo nane zinatoa maji vizuri na moja likisua sua.
Amesema mradi umesaidia kupunguza magonjwa yayokanayo na maji kama macho, upele, matumbo, typhoid na kupunguza umbali wa kutembea muda mrefu kutafuta maji.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA taifa Idrisa Mshoro amewataka wafanyakazi wa RUWASA wilayani humo kuhakikisha wanakamilisha upatikanaji wa pump na sola ili wananchi wapate maji kama ilivyotarajiwa na kwamba wauziwe maji kwa bei elekezi ya serikali inayotarajiwa kuanza Agosti 1, 2022 na kudumu kwa mwaka mmoja kabla ya marekebisho mapya.