skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki,Maswa

Mvua kubwa iliyoambatana na upepo na mawe imeezua mapaa ya nyumba 10 huku ikiangusha kuta za nyumba mbili katika mji wa Malampaka uliopo wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu.

Kufuatia mvua hiyo watu 51 ambao ni wakazi wa nyumba hizo hawana sehemu ya kuishi mara baada ya nyumba zao kuezuliwa paa na kuta kuanguka.

Akitoa taarifa mbele ya mkuu wa wilaya, afisa mtendaji wa kijiji cha Malampaka,Julius Mabondo amesema tukio hilo limetokea Februari 17 mwaka huu majira ya saa 9:00 mchana ambapo mvua hiyo ilinyesha kwa dakika 30 huku akiongeza kuwa hakuna taarifa ya kifo katika Maafa hayo.

Katika hatua nyingine Mabondo amesema licha ya mvua hiyo kuleta madhara imesababisha pia kuangusha transfoma ikiwa ni sambamba na kuathiri mazao mbalimbali yaliyoko shambani yakiwemo mahindi na Pamba huku akifafanua kuwa hadi sasa hakuna taarifa sahihi ni kiasi gani cha ekari kilichoathirika.

Mabondo amesema hadi sasa thamani ya athari iliyosababishwa na mvua hiyo bado haijafahamika na tathmini ya madhara hayo inaendelea kufanyika.

Aswege Kaminyoge ni mkuu wa wilaya ya Maswa amezitembelea kaya zilizopata maafa hayo na mbali na kuzipatia pole ameiagiza halmashauri ya wilaya hiyo kuhakikisha inatoa kiasi cha kilo gramu 60 za mahindi na mboga zikiwemo dagaa na maharage kwa kila kaya ambayo imeathirika ikiwa ni pamoja na kupatiwa hifadhi ya muda wakati wakiendelea na urekebishaji wa nyumba zao.

Pamoja na hayo ameuagiza uongozi wa halmashauri hiyo kufanya tathimini ya maafa hayo Ili kupata gharama halisi huku idara ya ujenzi akiitaka kutoa elimu juu ya ujenzi wa nyumba bora.

“Mkurugenzi wa wilaya halmashauri ya wilaya ya Maswa kwa kuwa serikali imetuletea mahindi ya bei nafuu hakikisha kwa msaada wa haraka hizi kaya zote zilizokumbwa na maafa kila moja inapata kg 60 ya mahindi pamoja na mboga ambazo ni dagaa na maharage, wapeweni hifadhi ya muda wakati wanarekebisha nyumbani zao na tathimini ifanyike kujua gharama halisi ya maafa haya ili serikali ione namna ya kuwasaidia, wataalam wa ujenzi toeni elimu kwa wananchi juu ya ujenzi bora wa nyumba,”amesema Kaminyoge .

Kwa upande wake diwani wa kata ya Malampaka Renatus Mashala kamshukuru mkuu wa wilaya kufika katika mji huo na kujionea maafa hayo huku akiishukuru serikali kwa msaada ambao utatolewa na kusisitiza kuwa watazisaidia kaya hizo ili ziweze kuishi kama ilivyokuwa awali.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma