skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na. Adela Madyane

Mtandao wa mawasiliano ya jamii Tanzania TZCNA kwa kushirikiana na Kituo cha Radio cha Buha FM Kasulu, wamezindua chumba cha kompyuta kwa ajili ya mtandao wa mawasiliano ya kidijitali kwa ajili ya jamii wilayani Kasulu kitakachotumiwa na wanachama wa mtandao na ushirika wa kidigitali Kasulu KACONECOS na wananchi mkoani Kigoma

Tukio hilo limefanyika jumanne November mosi mjini Kasulu mkoani Kigoma ambapo jumla ya kompyuta tano za kisasa zimeunganishwa kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha mfumo wa mawasiliano ya TEHAMA kwa wanachama na jamii mkoani Kigoma na kuchochea matumizi ya mawasiliano ya internet kwa wananchi.

Akizindua chumba hicho, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Bw. Joseph Kashushula amepongeza kuhusu uamuzi wa kuanzishwa kwa ushirika wa mitandao ya kijamii na huduma za kidijitali kwa jamii pamoja na ununuzi wa vifaa hivyo akihimiza vitumike kama chachu ya kuamsha ari ya jamii vijijini kutumia TEHAMA kama chanzo cha taarifa katika shughuli za maendeleo.

Bw. Kashushura amesisitiza kuwa, kutokana na mabadiliko ya kidigitali duniani, matumizi ya TEHAMA katika shughuli za kijamii hayakwepeki hivyo chumba hicho kiwe chachu kwa jamii ya wilaya ya Kasulu na mkoa wa Kigoma kuanza kujifunza na kutumia zana za kisasa za mawasiliano ya kidigitali.

Ndugu Joseph Kashushura (katikati) Kiteta jambo na Dkt Jabhera Matogoro, mkurugenzi wa Mtandao wa vyama vya ushirika wa kidijitali Tanzania (TZCNA) na Bi. Silesi Malli (kushoto) Mwenyekiti wa chama cha Ushirika wa kidigitali Kasulu (KACONECOS) baada ya kukata utepe wa kuzidua chumba cha kompyuta.

Aidha Kashushura ameahidi kusaidia kuongeza kompyuta zaidi katika kituo hicho cha mawasiliano ya jamii ili kupanua wigo zaidi kwa wanachama na jamii kukuza ujuzi katiak masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano ya jamii.

Wakati huo huo, Mtandao wa mawasiliano ya jamii Tanzania unaoundwa na vyama vinne vya ushirika wa mtandao wa kidijitali kwa jamii, Kasulu, Tarime, Nyansa na Kondoa, wamezindua kongamano la tatu la kitaifa la mjadala wa fursa na changamoto za matumizi ya internet kwa jamii sambamba na kuhimiza jamii kutumia mawasiliano kukuza uchumi.

Akitoa mada katika kongamano hili, Mtaalamu wa mawasiliano Tanzania na mwasisi wa mtandao wa kijamii Tanzania, ambaye pia ni mhazili wa chuo kikuu cha Dodoma Dk Jabela Matogolo ameitaka jamii kutumia huduma za mawasiliano  katika kujikwamua kiuchumi.

“ Lipo pengo la asilimia 40 la wananchi kushindwa kutumia huduma za mawasiliano zilizowekwa kwenye maeneo yao, hivyo ni jukumu la wanamtandao kuendelea kutoa elimu na kuwajengea wananchi hao uwezo wa kutumia miundombinu hiyo kwa maendeleo yao” Amesema Matogolo

Washiriki wa kongamano la tatu la kitaifa la kujadili fursa na changamoto za mawasiliano ya kijamii kidijitali, na matumizi madogo ya internet vijijini, linalofanyika mjini Kasulu mkoani Kigoma.

 Akiongea kwa niaba ya washiriki wengine wa mtandao mwenyekiti wa Kondoa Community Network Cooperative Society Salama Salum amesema  jamii inapaswa kuelewa vyema matumizi sahihi ya simu ganja katika kujiinua kiuchumi hasa wanawake na vijana ambao wanajua matumizi ya simu hizo kuwa ni kupiga picha za selfie, na kutupia kwenye mitandao ya kojamii ya facebook, whatsapp na instagram.

Naye mwenyekiti wa Kasulu  Community Network Cooperative Society Siles Malli amesema watoto waliopo mashuleni wanapaswa kupewa elimu sahihi ya matumizi ya vifaa vya kidigatali ikiwemo kompyuta ns kuvipata kwa gharama nafuu ili wajue manufaa yake na kuwawezesha zaidi kupenda shule na kupunguza utoro

Zaidi ya washiriki 40 kutoka mikoa ya Kigoma, Katavi, Dodoma, Ruvuma, Mara, Kagera na Dar es Salaam wameshiriki Kongamano hilo ambapo wakufunzi wa kimataifa kutoka Norway, Kenya na Uganda wametoa mada za umhimu wa matumizi ya internet kwa jamii duniani na fursa za kiuchumi kupitia mitandaoo ya kijamii.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma