skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Adela Madyane-Kigoma

MKUU wa wilaya ya Buhigwe Michael Ngayanila ametoa wito kwa taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali kuandaa matamasha mbali mbali ya kimichezo kwa lengo la kutambua vipaji vya vijana na kuviendeleza.

Aliyasema haya alipokuwa akizungumza na vijana katika bonanza la nikonekt lililofadhiliwa na shirika la umeme nchini (TANESCO), benki ya CRDB, shirika la THPS na wadau wengine lenye lengo la kuwakutanisha vijana na kubaini vipaji vyao sambamba na kutoa elimu juu ya huduma mpya ya nikonekt yaliyofanyika manispaa ya Kigoma ujiji katika viwanja vya jim carnal.

“Kigoma ni miongoni mwa mikoa yenye vijana wengi wenye vipaji, ila wengi hawajatambuliwa na kuendelezwa, naomba tamasha hili liweze kutoa fursa kwa wadau wengine kufunguka na kufanya matamasha kama haya ili kufungua na kuvisogeza mbele vipaji vya vijana vionekane na viwasaidie kusonga mbele katika maisha yao kwani michezo ni ajira na michezo ni kazi” Alisema Ngayanila.

Mkuu wa wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma Kanali Ngayalina (aliyevaa kofia) akikagua timu ya mpira ya Tanesco dhidi ya wapinzani wao CRDB

Akiongelea huduma mpya ya nikonekt alisema itasaidi kuendana na kasi ya dunia ya kidigitali kwani hakutakuwa na haja ya kutembea umbali mrefu wala kutumia gharama kubwa na kuwataka wananchi kutumia muda huo kufanya kazi kwani kulikuwa na upotevu wa rasilimali muda na pesa wakati wa kufanya ufuatikiaji wa umeme.

Kwa upande wake Jafari Mpina mkurugenzi mtendaji wa Tanesco Kigoma alisema vijana wengi hawapati nafasi ya kuonesha vipaji vyao ili viweze kuibuliwa na kwamba shirika lao linathamini michezo wakiamini kwamba michezo ni afya na burudani lakini pia husaidia kujenga mahusiano mazuri kati ya taasisi moja na nyingine pamoja na wateja wao.

Akizungumzia mfumo wa nikonekt alisema kwa mkoani Kigoma ulianza rasmi Juni 6, 2022 na kwamba hadi sasa wateja wengi wameufaika.

Akiongelea faida za mfumo huo amesema kuwa unamuwezesha mteja kupata huduma za Tanesco ndani ya muda na bila kupoteza gharama nyingi za usafiri pamoja na muda wa ufuatiliaji

“ Mfumo huu umetusaidia sisi kama shirika kwa kupunguza urasimu pamoja na vishoka waliokuwa wanawasumbua wateja mtaani na kuwatapeli, nawahakikishia wananchi kuwa kwa kutumia mfumo huu huduma za umeme zitapatikana ndani ya muda mfupi kwani vitendea kazi tunavyo vya kutosha na wafanyakazi tunao” Alisisitiza Mpina.

Naye Victor Bihemo mfanyakazi wa Tanesco ameziomba taasisi mbalimbali kuendelea kuwakutanisha wafanya kazi wao na wananchi ki michezo kwakuwa ni sehemu ya kuongea na wakurugenzi wao kwani wakiwa kazini hawakutani na hivyo kuwa ngumu kwa wao kubadilishana mawazo juu ya utendaji kazi wao

Vile vile afisa wa benki ya CRDB Mlokozi Emmanuel alisema bonanza za michezo huwasaidia kujenga mahusiano zaidi hivyo yaendelee kufanyika mara kwa mara

Akizungumza kwa niaba ya vijana Hussein Ramdhan alisema viongozi wa michezo mkoani wangalie namna ya kuratibu timu ya vijana ya mkoa ili vijana wengi wapate nafasi ya kuonesha vipaji vyao kwakuwa uwezo wanao lakini hawana timu na kwamba timu zilizopo zipo Ujiji pekee na sio Mwanga wala Kigoma mjini.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma