skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki ,Bariadi

Ukatili wa kijinsia umetajwa kuwa bado ni changamoto kubwa ndani ya  jamii  wilayani Bariadi mkoani Simiyu, huku ikielezwa kuwa jitihada zaidi zinahitajika ili kuhakikisha matukio hayo yanaripotiwa na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria ili kukomesha vitendo hivyo.

Hayo yamesemwa na  Frank Kasamwa ambaye ni mratibu mradi  wa kampeni ya kuimarisha usawa wa kijinsia mkoa wa Simiyu kwenye mkutano wa kutoa elimu ya kupinga ukatili ngazi ya jamii uliofanyika katika kata ya Dutwa wilaya ya Bariadi

Kasamwa anasisitiza kuwa vitendo vya ukatili kwenye jamii yetu vimeshamili kiasi cha kusababisha athali mbali mbali za kisaikolojia, kijami na hata kimwili kwa wanaofanyiwa ukatili huo pamoja na jamii zao.

“Tunapokuja kuimarisha usawa wa kijinsia lazima tuangalie makundi yote hasahasa mtoto, kuna mawakala wa mabadiliko ya tabia ngazi ya jamii hawa watatusaidia kuhakikisha wanawafundisha wazazi/ jamii kujua ukatili wanaoufanywa dhidi ya watoto wao”

Mratibu huyo anasisitiza kuwa ukatili upo wa aina tofauti tofauti  mbali na kuwapatia watoto  mimba kuna ukatili pia wa kuwakatisha watoto masomo yao na kuwalazimisha kwenda kuchunga mifugo

Bw. Frank Kasamwa (aliyesimama) Mratibu wa kampeni ya kupinga ukatili mkoani Simiyu akizungumza na wadau mbalimbali

“ukitembelea mighahawani, vituo vya mabasi na mitaani utakuta watoto wanajihusisha na biashara ndogondogo mfano kuuza karanga, mayai na matunda katika umri mdogo jambo linalopelekea wengine kufanyiwa ukatili ikiwemo kubakwa na kulawitiwa, tunataka tuwafundishe  watoto mbinu za kuripoti matukio ya ukatili ili wapate ujasiri”

Aidha Kasamwa alieleza kuwa taasisi ya Mass Media inatarajia kuanzisha klabu za kupinga ukatili mashuleni ambapo watoto watafundishwa mbinu za utoaji wa taarifa za ukatili na hatua zitachukuliwa na mamlaka mbalimbali ili kuwalinda watoto

Kwa upande wake katibu tawala wilaya ya Bariadi Nicodemus Shirima  amewataka wananchi kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hususan kwa watoto na badala yake wawe mabalozi wazuri wa kupinga vitendo hivyo ndani ya jamii na kwa kufanya hivyo vitapungua kwa kiasi kikubwa na hatimaye kutokomezwa. 

Katibu tawala wilaya ya Bariadi Nicodemus Shirima

” Ndugu zangu sisi ndio wa kwanza mradi huu umeanzia kwetu, na sisi tutakuwa mabalozi kwa wenzetu kwasababu tumeambiwa kuna ukatili wa aina nyingi …hata wazazi kutokuchangia chakula cha watoto wao shuleni ni ukatili..we fikiria mtoto mdogo ameamka asubuhi sa nyingine usiku hakula vizuri alafu ameenda shuleni amekaa mpaka jioni hajala alafu unataka asome vizuri inawezekana hiyo kitu..onesha upendo kwa mtoto bila masharti na ukionesha upendo kwake bila masharti ina maana unamjengea kujiamini na pia unamuondolea ukatili wa kijinsia”  amesema Shirima na kuongeza kuwa:

” Kutokupeleka watoto shule ni ukatili …unasema mimi nitasomesha mtoto wa kiume tu wa kike sitamsomesha huo ni ukatili..kuna wengine wanawachukua watoto wanaenda nao mnadani kuwasaidia biashara huo nao ni ukatili ” ameongeza

Isabela Nyaulingo ni afisa tarafa ya Dutwa amewaasa wazazi kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hususan kwa watoto na badala yake wawe chachu ya mafanikio ya watoto hao kitaaluma huku Pastory Msilanga ambaye ni afisa elimu kata  hiyo  (Dutwa) akisisitiza ufuatiliaji wa kesi za ukatili wa kijinsia zinazoripotiwa ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wahusika.

“Ule mtindo wa kuozesha watoto tuuache ule mtindo wa kusema huyu mtoto mwenyewe hataki shule tuuache tuingie kwenye ushindani wa kitaaluma sawa na mikoa mingine ..kina mama tuwe chachu ya kuwaamasisha watoto wetu kwenda shule watoto wa kike wengi wanafanya biashara humu na tunawaona kule kwenye biashara ndiko wanakutana na vishawishi   ” amesema Nyaulingo

Mradi huo wa kampeni ya kuimarisha usawa wa kijinsia mkoa wa  Simiyu  unatekelezwa kwenye kata sita katika wilaya za Bariadi na Busega chini ya ufadhili wa FCS kwa kipindi cha miezi nane  kuanzia Septemba 2022 mpaka Aprili 2023 kupitia  asasi  ya kiraia ya Mass Media ambapo shughuli mbalimbali  zinafanyika  ikiwemo kutoa elimu ili kuhakikisha vitendo vya ukatili vinaripotiwa na wahusika kuchukuliwa hatua..

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma