skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Na Anita Balingilaki, Simiyu

Askari mmoja wa jeshi la polisi anatuhumiwa kumpiga na kumjeruhi vibaya mwanaye wa kumzaa na kumsababishia majeraha makubwa na maumivu makali mwilini mwake, kitendo kinacho laaniwa na wananchi, wanaharakati na jamii kwa ujumla .

Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Simiyu Blasius Chatanda amesema jeshi hilo tayari  linamshikilia askari polisi mwenye no H.4178 PC  Abati Benedicto Nkalango kwa tuhuma za kumjeruhi mtoto wake mwenye umri wa miaka saba mwanafunzi darasa la kwanza shule ya Herbeth Gappa English mediam na tukio hilo limetokea  Jan 15, 2023 majira ya saa 11:00  asubuhi katika kambi ya kituo cha polisi Bariadi.

“Imeonekana picha kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha mtoto anayedaiwa kujeruhiwa  na baba yake mzazi ambaye ni askari..mnamo Jan 15,2023  siku hiyo mtuhumiwa alikuwa nyumbani kwake alikagua madaftari ya mtoto huyo na kugundua alikuwa amekosa baadhi ya mazoezi ya hisabati aliyokuwa amekosa shuleni…alimchapa viboko vingi ambavyo hakumbuki  idadi na  kumsababishia kutokwa damu maeneo ya mgongoni” amesema Kamanda Chatanda na kuongeza kuwa:

” Mtuhumiwa baada ya kufanya ukatili huo alichukua dawa na kumpatia matibabu akiwa nyumbani.” ameongeza kamanda Chatanda.

Wananchi mkoani Simiyu wamelaani kitendo cha baba kumpiga mwanae na kumsababishia majeraha huku wakilipongeza jeshi la polisi mkoani humo kuchukua hatua dhidi ya mtuhumiwa wa tukio hilo.

Wamesema hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake ili ikawe fundisho kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kwani wapo ambao kwa namna moja ama nyingine ufanya matukio/vitendo  kama hivyo kwa kujificha na kuamini hawawezi gundulika kirahisi.

*Namna tukio lilivyogundulika*

Bernadeta Katendele ambaye ni mwalimu wa mwanafunzi huyo jina (linahifadhiwa) anasimuli kuwa yeye anafundisha darasa la kwanza A na B masomo ya kusoma na kuandika  na kwamba walipofungua shule Jan 9, 2023 mtoto huyo aliripoti na alikuwa na mahudhurio mazuri siku ya jumatano january 11, akaanza kupata shida.

“mimi nikahisi kwamba labda ana tatizo la “sickle cell” akawa ni mtu wa kulala lala tu darasani…siku ya jumatano ya wiki ya pili tangu kufungua shule mtoto huyu hatukumuona kumbe ndio alizidiwa nikaangalia anapokaa haonekani, siku ya alhamisi ndio alikuja kilikuwa kipindi changu cha kwanza akawa amelala kila ukimfatilia anaandika lakini huku analala badae nikamfata mpaka kwenye dawati lake nikaanza kumuuliza kirafiki anaumwa nini akasema ” mimi nilianguka kwenye mlango nikakanyaga maji ya moto kwahiyo niliangukia kichwa na mgongo wote umeungua  ” anasimulia mwl huyo.

Picha ya mtoto aliyejeruahiwa vibaya kwa kipigo kinachotajwa kutekelezwa na baba yake mzazi ambaye ni askari wa Jeshi la Polisi

” Sasa nikamwangalia kwenye sikio alikuwa na jeraha lile jeraha likanitisha nikasema mhhh! maji gani mpaka kwenye sikio ikabidi nianze kuuliza vizuri akasema ” hata ukiniangalia kwenye shati utaona damu” sasa ikanishtua nikampeleka ofisini kwetu tuna godoro la wagonjwa mtoto akaja akalala lakini lala yake ni ya shida analala kifudifudi ikabidi nimuite matroni nikamwambia ebu tumuangalie huyu mtoto, tulipomuangalia mgongoni tukagundua sio maji bali majeraha kama alikuwa anapigwa na ncha kali tukamuita mzazi wake alivyofika mama yake ananiambia mimi ni shangazi yake lakini badae tukagundua ni mama yake wa kambo tukataka kujua ilikuwaje akawa hivi akasema  baba yake uwa anampiga  anapokuwa anamfundisha alimpiga siku hiyo aliposhindwa kusoma “E” yaani E tu ambayo ndio siku ya tatu ya wiki la kwanza basi tukamuuliza wakati anampiga ulikuwa wapi akajibu baba yake ni mkali”anaendelea kusimulia.

Mwl huyo anasema wakaamua kuitana wote hatua iliyopelekea mwanamke kugundua na kumpigia mme wake” mme wake akamwambia wamekunyima mtoto nikaichukua ile simu nikamwambia tunakaa kikao huyu mtoto uwa anakuja na basi mpaka tukae kikao ndio tumkabidhi mama yake ila lengo letu ni tuweze kubaini tunafanya nini kumsaidia mtoto…kikao kilivyoisha akaja mhasibu wa parokia akasema twendeni polisi mambo haya yakajibiwe polisi mke wake akaanza kusema “mgemsamehe” tukamwambia nenda na wewe polisi ili ukajibu basi akaondoka mke wake hana amani”

Kuhusu maendeleo ya mtoto shuleni mwl wake anasema yupo vizuri na kazi zake zinaridhisha hata kwa kuziangalia ikiwemo  kusoma kuhesabu na kuandikia huku akitoa ushauri kwa walimu, wazazi na jamii  kuona mtoto wa mwezio kuwa ni wako  na mtu aonapo hali ya tofauti lazima amsogelee na kujua tatizo ili litatulike kwa haraka.  

Dkt Emmanuel Costantine ni mganga mfawidhi wa hospitali ya halmashauri ya mji wa Bariadi anasema Jan 19,2023 majira ya saa 4:00 asubuhi walimpokea mtoto huyo ( jina linahifadhiwa ) akiwa na majeraha kwenye mgongo nyuma ya sikio  majeraha hayo mengine ya zamani mengi mapya huku akiongeza kuwa hali yake kwasasa inaendelea vizuri baada ya kupata matibabu na amelazwa kwenye wodi ya watoto akiendelea na matibabu.

Sababu za mama wa mtoto huyo kutengana na baba yake

Naomi Kaliwa ni bibi wa mtoto huyo amesema awali askari huyo alikuwa anapanga kwenye nyumba yake na akiwa hapo alimpatia ujauzito binti.

“Siku moja akaniambia anaumwa nikampa hela ya kwenda kupima nijarudi jioni akaniambia ana mimba ya huyo askari ..huyo askari akawa hajui kama mi ninajua hiyo taarifa ikatokea siku ikabidi tumuite na mzee wangu tukivyomuuliza akajibu ni kweli ujauzito ni wake tukamtaka atoe huduma kwa mwanetu na ikabidi tumuambie amuoe askari akatujibu serikalini maaskari  hawaruhusiwi kuoa mpaka ipite miaka mitatu nikamuuliza kama alijua hivyo kwanini alimpatia mimba mwangu” anasema mama huyo na kuongeza kuwa:

“Badae akaikataa mimba binti yangu na mimi tukaenda polisi tulivyofika pale akaikataa mimba tukaacha na kuona hatuwezi kumlazimisha nikalea  mimba mpaka akajifungua tukakaa nae muda mrefu badae akaanza kuhudumia kidogo kidogo  siku  moja akaja kwangu kwa lengo la kumchukua mtoto kwenda kumnunulia nguo nikakubali lakini chaajabu hakumnunulia nguo  akamrudisha hivyo hivyo kesho yake akarudi tena kwa lengo lile lile la kumnunulia nguo nikamkatalia kwa kuwa nilikuwa nasafiri kwenda Sumbawanga akanibembeleza anaenda kumnunulia nguo na  kumrudisha nikamkubalia chaajabu hakumrudisha mtoto kumbe kesho yake akamsafirisha mpaka Runzewe, ikabidi mi niende Sumbawanga kuhudumia mgonjwa nilikaa huko miezi miwili nikarudi Bariadi nilipoenda kufatilia mtoto akawa mkali nikamuacha akae nae. Anasimulia mama mzazi wa mtoto huyo.

Imebainika kuw amama yake mzazi alipokuwa akitaka kumuona mzazi mwenzake anakataa ikabidi arudi kasori anapofanyia kazi ikawa kimya mpaka Jan 23,2023

“Nilikuwa naenda shamba ndio mtu akanipigia simu kunieleza taarifa za kupigwa kwa mjukuu wangu ndio nikafika hospitali naiomba serikali uchukie hatua dhidi yake ukiangalia kazi anayoifanya ni ya kulinda watu na mali zao..kingine naiomba serikali inikabidhi mjukuu wangu  nimlee aendelee kusoma alipokuwa anasoma” anaelezea bibi huyo.

 Kwa upande wake afisa ustawi wa jamii kutoka halmashauri ya mji wa Bariadi Janeth Jackson amesema tukio hilo wamelipokea siku ya alhamisi majira ya 4:00 asubuhi kutoka kwa daktari alipolazwa mtoto huyo na tayari alikuwa wodini na wao  (ustawi wa jamii)  watahakikisha mtoto anatibiwa na kupata matibabu stahiki.

Aidha Jackson amesema wamegundua ulinzi na usalama wa mtoto haupo na  wanachokifanya wao (ustawi wa jamii) ni kuchunguza ili kujua ndugu wa mtoto  upande wa mama na baba wako wapi kwasasa maana taarifa walizozipokea ni kuwa mama na baba hawaishi pamoja na awali mtoto alikuwa anaishi kwa babu mzaa baba na badae baba yake alimfata Disemba 2022   kwaajili ya kuja kuanza shule na kwa kipindi hicho kifupi ndio wakapokea taarifa za ukatilii huo.

” Tukipozungumza na mtoto alituambia alipigwa siku ya jumapili na jumatatu akwenda shule jumanne akaenda shule lakini walimu hawakujua jumatano hakwenda alhamisi alikwenda na ndipo mwalimu wake akagundua kuna tatizo…tumelipokea kwa maskitiko makubwa na mtoto alikuwa na majeraha makubwa sana  mpaka sasa tunachoendelea nacho ni kutafuta mama yake yupo wapi babu yake kizaa baba  tayari ameshakuja na tumezungumza nae na amekiri wazi tupo tayari kukaa na mtoto lakini bado sisi uchunguzi wetu unaendelea ili tujue mazingira rafiki ya mtoto kuishi ni yapi kati ya mama bibi mzaza mama au babu mzaa baba na tutatoa taarifa” amesema Jackson

Mbali na hayo afisa huyo amesema  matukio ya ukatili kwa mwaka 2022  yalikuwa 595 na tangu  mwaka huu uanze  tukio hilo ni la kwanza  huku akitoa ushauri kwa jamii kuachana na vitendo vya ukatili na kuwafichua wale wote wanaotenda vitendo hivyo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kampeni ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii  (SMAUJATA)  mkoa wa Simiyu Lameck Mapalala amesema suala la ukatili ni jambo lisiloweza kuvumilika kwani linaathari kubwa huku akiiomba  jamii iendelee kutoa ushirikia no wa  kufichua vitendo hivyo vya kikatili ili sheria ichukue mkondo wake hatua itakayopelekea ustawi  chanya na maendeleo endelevu.

Kwa mujibu wa sheria ya mtoto kuhusu ulinzi dhidi ya mateso na udhalilishaji  kifungu cha 13 (1) mtu hatamsababishia mtoto mateso au aina nyingine ya ukatili, kumpa adhabu zisizo za kibinadamu au kumdhalilisha mtoto ikijumuisha mila na desturi zozote zenye madhara kwa mtoto kimwili au kiakili. (2) Adhabu haitakuwa stahili kwa mtoto iwapo ni mbaya kwa aina yake au ni kubwa kwa kiwango chake kulingana na umri wa mtoto, hali ya mtoto kimwili na kiakili na adhabu haitakuwa stahili  kwa mtoto  iwapo kutokana na umri mdogo wa mtoto au kwa sababu nyingine hawezi kuelewa lengo la adhabu hiyo.

Udhalilishaji” ni instilahi kama ilivyotumika katika kifungu cha 3 cha sheria, maana yake kitendo  kinachofanywa kwa mtoto kwa nia au dhamira ya kumdhalilisha au kushusha hadhi yake. Mtu atakayekiuka  kifungu chochote katika  sehemu hii atakuwa ametenda kosa na atakapitiwa hatiani  atalipa faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo   cha miezi isiyozidi sita au vyote kwa pamoja.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma