skip to Main Content
Simu: +255 653 200 211 | Barua Pepe: info@buhafmradio.co.tz  

Adela Madyane- Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Lameck Mlacha amewataka wadau wa haki kutotumia adhabu mbadala katika mazingira ya kuishangaza jamii kwani matumizi ya adhabu hiyo sio matakwa ya mtu binafsi wala taasisi bali ni matakwa ya kisheria.

Mlacha alitoa wito huo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kuanzia tarehe 29 Julai 2022 yaliyoandaliwa na wizara ya mambo ya ndani- idara ya huduma za uangalizi mkoa wa Kigoma yaliyowashirikisha wadau kutoka mahakama, ofisi ya taifa ya mashtaka, huduma za uangalizi, polisi, magereza na ustawi wa jamii.

“Adhabu mbadala haitakiwi kutolewa kiholela kwani inaweza kuharibu jamii, adhabu ya  kifungo chini ya miaka mitatu sio kigezo pekee, zingatieni aina ya kosa lililotendeka, jamii ina mtazamo gani na tabia za mhusika, na lazima kuzingitia kanuni na taratibu za kisheria” alisema Mlacha

Jaji mfawidhi aliongeza kuwa utekelezaji wa adhabu mbadala utawaepusha wahalifu wa makosa madogo kuiga tabia mbaya kutoka kwa wahalifu sugu waliopo gerezani, itapungunguza msongamano na gharama za kutunza wafungwa gerezani na kuwasaidia kukaa na familia zao na kutekeleza wajibu wao wa kifamilia na kijamii

“ Jamii itashiriki katika urekebishaji wa tabia za wahalifu na kunufaika moja kwa moja na shughuli wanazozifanya na pia kuwezesha utengamanisho wa wafungwa na jamii na kwamba kwa siku muhalifu atatakiwa kutoa muda wa masaa manne na kufanya kazi katika ofisi za umma na jamii bure” Alisisitiza Mlacha

Naye Mkurugenzi msaidizi wa idara ya huduma za uangalizi, Charles Nsanze alisema kuwa mafunzo hayo  yatakuwa chachu ya kutoa msukumo mpya wa utekelezaji na usimamizi wa adhabu hiyo kwa kusaidia kujenga uelewa wa pamoja juu ya utekelezaji wake na taratibu za kisheria katika utoaji wa adhabu hiyo

“Mkoa wa Kigoma una idadi ndogo ya wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje, kwa mwaka 2021 wafungwa 20 tu walitumikia adhabu hiyo, tumeona ni wachache na kwa pamoja kama wadau wa haki jinai tumeamua ili kujua wapi tunakwama na kutatua ili idadi iongezeke” Alisema Nsanze

Alisema kama wizara wanatafakari namna ya kuanza kuwapa likizo wafungwa wanaokaribia kumaliza vifungo vyao ili kupunguza wimbi la uharifu wa kujirudia kwakuwa wamekuwa wakiachiwa huru na baada ya wiki moja wanarudishwa tena gerezani

“Tunataka kuwaachia taratibu ili waone mabadiliko yaliyopo nje na kuondoa migogoro ya kifamilia pia, na tunawaza tuanze kuwalipa sehemu ya fedha walizotumikia kipindi chote walichokuwa gerezani ili kuwapatia mtaji wanaporudi uraiani, tutaanza kuwapatia masaa 48 mpaka 72 kama likizo ya kujitengeneza mazingira ya kukaa uraiani” alisema Nsanze

Kwa upande wake afisa ustawi wa jamii mkoa Petro Mbwanji alisema adhabu mbadala zinasaidia familia kuondokana na hali ngumu kiuchumi pindi inapotokea mzazi mmoja anakuwa yupo jela ila kwa kifungo hicho ataweza kufanya kazi na kusaidia familia yake na jamii kwa ujumla

“Tunafuatilia kesi za wafungwa chini ya miaka mitatu, kama hawajatoka tunawafuatilia na magerezani ili waweze kurudi mtaani kufanya shughuli za kimaendeleo, tunawachukua ambao hawana madhara katika jamii pamoja na makosa waliyofanya“ Alisema Mbwanji

Akizungumza kwa niaba ya jamii Costantino Kazabura alisema adhabu mbadala sio mbaya ila mamalaka zijikite kuhakikisha wanaorudishwa hawataleta au kuletewa madhara kutokana na aina ya kosa walilofanya.

Kwa upande wa Shirika la umoja wa mataifa linalohudumia wakimbizi (UNHCR) ambao ndio wafadhili wa mafunzo hayo, Rehema Msami afisa hifadhi mshiriki alisema walifadhili mafunzo hayo kwakuwa adhabu mbadala zinawagusa pia wakimbizi ambao wapo chini na wangependa nao wanufaike na sheria ya adhabau mbadala kwasababu wanaongozwa ya sheria ya nchi ya Tanzania kwahio na kwamba itawapasa kuandaa taratibu za vibali vya kufanya kazi nje ya kambi.

Mafunzo hayo yanalenga kutekeleza maelekezo ya jaji mkuu wa Tanzania,Ibrahim Juma ambayo amekuwa akiyatoa  kwa nyakati tofauti  akihimiza matumizi ya adhabu mbadala kwa wahalifu wasio hatarishi kwa usalama wa raia na mali zao, huku akiwataka wadau kutekeleza adhabu hiyo kwa wahalifu wote waliotimiza vigezo vya kisheria.

Back To Top
Buha FM · Buha FM Radio Sauti Ya Kigoma